Elimu suluhu ya migogoro ndani ya Simba na Mzee Kilomoni

170

Maisha yanaenda kasi sana. Hii inapelekea hata kuibuka na semi za Waswahili kuwa “Mambo ni mengi muda mchache” inatoa tafsiri ya mwendo wa muda na mambo yanayotendeka katika kipindi hicho.

Siku za hivi karibuni limeibuka suala lililovuta na linalovuta hisia za mashabiki na wapenda soka nchini Tanzania kutokana na hati ya klabu ya Simba kumilikiwa na Mzee Hamis Kilomoni hivyo Simba haiwezi kukabidhiwa muwekezaji bila kuwepo vitu vya msingi hati ikiwemo.

Kama hujui, wacha nikukumbushe kidogo juu ya jambo hili. Baada ya Simba kumkabidhi Mohammed Dewji “MO” timu kama muwekezaji kwa asilimia 49 zinazobaki kwenda kwa wanachama na MO kukubali kuweka bilioni 20 kama sehemu ya uwekezaji huo kilichokuwa kimebaki ni mda tu wa jambo hilo kutokea.

Sasa wakati likisubiliwa la MO kuweka fedha, akaibua maombi ya kutoweka hizo pesa bila kupewa hati ya jengo la Simba katika kuulizana hati ipo kwa aliyekuwa kwenye baraza la wadhamini Mzee Kilomoni. Kilomoni akagoma kutoa kwa madai ile ni timu ya wanachama.

Hapa ndipo pameibua kalamu yangu. Hivi sasa asilimia kubwa ya Wanasimba wanamchukia Kilomoni wakiamini anakwamisha mafanikio ya Simba wengine wakiona kama ana unazi wa timu mbili, yote yanasemwa lakini ukweli uko wapi juu ya hili.

Inawezekana wote wapo sahihi katika hilo. Kikubwa wakati mfumo huu mpya wa uendeshaji timu unaingia uliacha makundi mawili yaliyotofauti katika utambuzi na uelewa tofauti, na hapa ndipo tatizo lilipo.

Naamini kuwa endapo watu kama Mzee Kilomoni wangekuwa wamepatiwa elimu juu ya uwekezaji na uendeshaji wake, changamoto hizi zisingetokea. Kumbuka suala kama hili limewai kutokea hata Yanga kupitia Mzee Akilimali aliyekataa uendeshwaji mpya wa klabu hiyo, yote ni ukosefu wa ufafanuzi wa namna klabu itaendeshwa na faida zake.

Lakini kuwe na uhakika wakati elimu hii inatolewa makando kando yanayojitokeza katika safari ya mfumo mpya yanaisha, ili isije kuwa mto mdogo unazimwa wakati ambao moto mkubwa una washwa katika tukio moja.

Anachokiona Kilomoni ni klabu ya maisha yake inaharibiwa na watu wachache hayuko tayari kuliona hilo. Elimu sio jambo la kubeza katika hili ndio maana ukisikia hata mijadala ya wanamichezo nchini bado utaona kuna tatizo katika uelewa wa misingi ya uwekezaji.

Ilitakiwa wakati Simba inafikia hatua mabadiliko haya angalau asilimia 95 wana uelewa sawa kuhusu uwekezaji na mabadiliko.

Maji yameshamwagika hayazoleki, lakini kwa hili yatazoleka tu kwa sababu utofauti wa uelewe huu utaendelea kuwa kikwanzo kikubwa hata kama hatakuwepo Mzee Hassan Kilomoni. Wengi wanaona klabu ina milikiwa na mtu mmoja badala ya uanachama waliouzoea mda mrefu. Wanajiona wanatengwa.

Ili maji yazoleke elimu ni nguzo kuu. Njia za elimu ni nyingi kupitia vyombo vya habari ambavyo bila shaka vina ushirkiano mzuri pamoja na kufanyika mikutano ya kanda katika mikoa ya Tanzania. Mikutano itakuwa na lengo moja tu Simba mpya katika uwekezaji.

Author: Asifiwe Mbembela