Samatta kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi ya Mabingwa

Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars” Mbwana Ally Samatta na mchezaji wa klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji anatarajia kuandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo klabu yake ya Genk imesafiri kucheza na Red Bull Salzburg ya Austria katika dimba la Wals-Siezenheim kwenye mashindano hayo.
Samatta ambaye ni kinara wa ufungaji magoli Genk kwenye Ligi ya Ubeligiji (5) endapo atacheza mchezo wa leo atakuwa Mtanzania wa kwanza kuwa sehemu ya kikosi katika michuano mikubwa upande wa ngazi ya vilabu Ulaya.
Kabla ya leo, ilikuwa haifahamiki kama angecheza leo kutokana na majeraha aliyoyapata akiwa na kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania wakicheza na Burundi kusaka nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia lakini ripoti ya Madaktari imeondoa shaka juu ya hilo.
‘Samagoal’ amejumuishwa kwenye kikosi kilichosafiri kwenda Austria kuivaa Red Bull Salzburg timu hiyo mchezo utakaopigwa majira ya saa 4 za usiku majira ya Afrika Mashariki.
Mbwana Ally Samatta atakuwa mchezaji wa tatu Afrika Mashariki kucheza mashindano hayo baada ya MacDonald Mariga (2010) na Victor Wanyama wa Kenya aliyecheza michuano hiyo akiwa na Tottenham Hotspurs.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends