Kaze ajigamba kuwajua Mtibwa Sugar kumeipa Yanga ushindi muhimu wa 1-0 VPL

Mwalimu wa Yanga, Cedric Kaze amesema kuwa ushindi walioupata mbele ya Mtibwa Sugar umetokana na kuwasoma wapinzani hao kwa muda mrefu ndani na nje ya uwanja.

Jana Jumamosi, Februari 20 Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Mkapa.

Bao pekee la ushindi lilipachikwa na kiungo Carlos Carlinhos ambaye alitokea benchi na kufunga bao hilo dakika ya 73 akimalizia pasi ya Tuisila Kisinda.

Ushindi huo unaifanya Yanga kujenga ngome nafasi ya kwanza ikiwa na jumla ya pointi 49 baada ya kucheza jumla ya mechi 21.

Kaze amesema: “Niliwasoma wapinzani wangu kupitia mashindano ya Kombe la Mapinduzi yaliyofanyika visiwani Zanzibar ambapo nilijua wapi nitaweza kupata ushindi juu ya kikosi hicho.

“Niliwaambia wachezaji wangu kwamba ni lazima wapambane na watumie akili kusaka ushindi kwa kuwa wachezaji ambao wanacheza nao wana uzoefu na uwezo wa kusaka ushindi ndani ya uwanja.

“Katika hilo tumefanikiwa na kushinda hivyo ni mwendelezo wetu wa kuyafuata mafanikio ndani ya uwanja,” amesema.

Mtibwa Sugar ambayo mchezo wake uliopita ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Ihefu imepoteza mbele ya Yanga ambayo ilitoka kulazimisha sare ya kufungana mabao 3-3 dhidi ya Kagera Sugar.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares