Dortmund yatimba fainali Kombe la Ujerumani, yaichapa Holstein Kiel 5-0

Borussia Dortmund wameitandika timu ya daraja la pili Holstein Kiel bao 5-0 na kufuzu hatua ya fainali ya Kombe la Ujerumani na sasa watachuana vikali na RB Leipzig.

Dortmund wameandikisha rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufunga goli tano kipindi cha kwanza katika michuano ya Kombe la Ujerumani nusu fainali, hata hivyo hawakuweza kuingia kambani tena katika kipindi cha pili.

Magoli ya Dortmund yalifungwa na Giovanni Reyna aliyefunga goli mbili, kiungo mshambuliaji Marco Reus, Thorgan Hazard na Jude Bellingham.

Jadon Sancho alikuwa mtoa msaada baada ya kutoa asisti 2 kwa Reyna na goli la kiungo mkabaji wa England Jude Bellingham.

Hata hivyo, walikuwa bila huduma ya mshambuliaji Erling Braut Haaland 20, raia wa Norway.

Fainali ya Dortmund inakuja kufuatia RB Leipzig kushinda mechi ya kibabe dhidi ya Werder Bremen katika dakika za ziada.

Historia kuandikwa kwenye fainali hiyo ambapo walimu wa timu hizo wataachana na timu zao mwishoni mwa msimu huu, Edin Terzic ataondoka Dortmund akimpisha Marco Rose.

Julian Nagelsmann anaondoka akimpisha Jesse Marsch na kujiunga na Bayern Munich.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares