Nuno asema Harry Kane haondoki Spurs

 

Kocha mpya wa Tottenham Nuno Espirito Santo amesema mshambuliaji wa timu hiyo Harry Kane ni mchezaji wao na atazungumza na mchezaji huyo kuhusu kurejea klabuni hapo.

 

Mshambuliaji Kane, 27, alikuwa kwenye matamanio ya kuondoka katika klabu ya Spurs na kwenda kwingineko ambapo mpaka sasa kocha Nuno amemwekea ugumu.

 

Kane kwa sasa anaendelea na mapumziko baada ya kukiongoza kikosi cha England kufika fainali ya Euro 2020 kabla ya kupoteza mtanange dhidi ya Italia kwenye mikwaju ya penati.

 

“Muda huu ni wake aendelee kupumzika na kupata nguvu mpya. Na baadaye nitazungumza naye”, alisema kocha huyo wa zamani wa Wolves.

 

Mwezi uliopita Mabingwa wa Ligi Kuu England klabu ya Manchester City ilikuwa imepiga hatua kubwa kuwania saini ya mshambuliaji huyo lakini kwa sasa ugumu unaonekana kuzaliwa upya.

 

Baadhi ya ripoti zimekuwa zikiripoti kuwa Kane aliomba kuondoka Tottenham mwishoni mwa msimu uliopita.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends