AC Milan, Inter zapambana kuufanikisha ujenzi wa uwanja mpya

Vilabu vya AC Milan na Inter Milan vinafanya mazungumzo ya kujaribu kutatua mzozo kuhusu mipango ya kujenga uwanja mpya kuchukua nafasi ya dimba la San Siro ambalo limekuwepo kwa karibu karne moja. AC Milan inayomilikiwa na kampuni ya Marekani ya Elliott na Inter Milan inayomilikiwa na kampuni ya China ya bidhaa za kieletroniki Suning, mwezi Julai viliwasilisha ombi la kujenga uwanja mpya wa pamoja wenye viti 60,000 katika eneo la San Siro.

Uwanja huo mpya ndio wazo muhimu katika mpango mpana wa miundo mbinu ya eneo hilo, ambao unajumuisha kuubomoa uwanja wa kihistoria wa San Siro, unaofahamika kama ‘La Scala del Calcio.‘

AC Milan na Inter zinauona uwanja mpya na wa kisasa kuwa njia muhimu ya kuimarisha mapato yao, ambayo yanabaki nyuma ya wenzao ambao wanamiliki viwanja vyao vya nyumbani, kama vile mahasimu wao wa Serie A Juventus FC na vilabu vingine vikuu UIaya.

Lakini manispaa ya Milan, ambayo inamiliki San Siro na inapaswa kutoa idhini yake kwa mpango huo, haijaonyesha nia ya kuuidhinisha mradi huo wa euro bilioni 1.2.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends