AC Milan yaendelea kuongoza kileleni licha ya kugawana pointi na Roma kufuatia sare ya 3 – 3

Klabu ya AC Milan imeangusha alama kwa mara kwanza msimu huu ndani ya Serie A baada ya Jana Jumatatu kutoshana nguvu na AS Roma kufuatia sare ya bao 3-3. Mshambuliaji wa zamani wa Barcelona na Manchester United Zlatan Ibrahimovic alitupia bao mbili ambazo hazikutosha kuipa alama zote tatu.

Ibrahimovic mwenye umri wa miaka 39, aliitanguliza Milan kabla ya Edin Dzeko kusawazisha bao hilo. Alexis Saelemaeker alirudisha uongozi kwa Milan lakini muda mchache tena Jordan Veretout akarudisha usawa wa magoli kwa kufunga upande wa Roma, saizi ikawa 2-2.

Ibrahimovic akafanya 3-2 akifunga kwa njia ya tuta lakini Marash Kumbulla akasawaziaha baadae. Matokeo hayo yanaifanya Milan kuendelea kuongoza msimamo wa ligi kuu nchini Italia Serie A kwa tofauti ya alama mbili mbele ya Napoli.

Licha ya umri wake, mbali na kukosa baadhi za mechi kutokana na kukutwa na dalili za Covid-19, lakini strika huyo wa Sweden na Milan Ibrahimovic amefunga goli sita katika michezo mitano pekee.

Mapema Jumatatu, Milan ilitoa taarifa kuwa kipa wake nambari moja Gianluigi Donnarumma amekutwa na maambukizi ya virusi vya Corona na nafasi yake kuchukuliwa na mkongwe Ciprian Tatarusanu.

Author: Asifiwe Mbembela