AC Milan yatimuliwa Europa League

Olympiakos Piraues ilipata ushindi wa kushangaza wa 3-1 katika Europa League dhidi ya AC Milan na kuwaweka katika hatua ya 32 za mwisho na kuwabandua nje Wataliano hao wakati nafasi za mwisho za hatua ya mtoano zilichukuliwa Alhamisi.

Mabao yote ya mechi hiyo nchini Ugiriki yalipatikana katika kipindi cha pili cha kusisimua, ambapo beki wa Milan Cristian Zapata alijifunga langoni mwake na kuipa Olympiakos uongozi wa 2-0 katika dakika ya 70 kabla ya kufunga moja na dakika chache baadaye na kuipa matumaini Milan.

Lakini uzembe wa ulinzi wa Milan ukaadhibiwa wakati Konstantinos Fortounis alipofunga penalti katika dakika ya 81 na kuipa timu yake ushindi ambao uliwaweka nafasi ya pili ya Kundi F na pointi 10. Hivyo walifuzu pamoja na vinara wa kundi hilo Real Betis, kwa kuwapiku mabingwa hao mara saba wa Ulaya kwa tofauti ya mabao.

Chelsea ilitoka sare ya 2-2 na Vidi FC mjini Budapest, wakati Malmo ya Sweden ikishinda 1-0 dhidi ya Besiktas na hivyo kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Genk katika Kundi I:

Bayer Leverkusen iliibomoa AEK Larnaca 5-1 na kumaliza kileleni mwa Kundi A, huku FC Zurich ikiimaliza nafasi ya pili baada ya sare ya 1-1 na Ludogorets.

Washindi wa Kundi C Zenit St Petersburg walizabwa 2-0 na Slavia Prague, ambo walinyakua nafasi ya pili na hivyo kuukosesha maana ushindi wa Bordeaux wa 1-0 dhidi ya FC Copenhagen kwa sababu timu zote zilibanduliwa nje.

Celtic waliochapwa 2-1 na Salzburg ambao walikuwa tayari wamekamata nafasi ya kwanza ya Kundi B, walihitaji msaada kutoka kwa Rosenborg. Wanorway hao walitoka sare ya 1-1 na RB Leipzig na kuwatimua nje wajerumani hao na kuwapa kibali Celtic.

Licha ya kuzabwa 3-0 na Sevilla,Krasnodar ilifuzu kutoka Kundi J kwa sababu Standard Liege iliweza tu kutoka sare tasa na Akhisar.

Watajiunga na Villarreal, Rapid Vienna, Dynamo Kiev na Stade Rennais, kwenye droo ya hatua ya mtoano Jumatatu wiki ijayo

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends