Adhabu kali yatungwa dhidi ya mashabiki watukutu EPL

Mashabiki watakaoenenda kinyume na utaratibu kwa wachezaji, mashabiki wenza, viongozi wa klabu au waamuzi watafungiwa na vilabu vyote vya EPL.

Katika kikao kilichofanyika leo Alhamisi Jijini London viongozi wa vilabu vya EPL kwa pamoja wamekubaliana kuwa shabiki yeyote atakayefungiwa na timu moja atakuwa amefungiwa na vilabu vyote 20.

Kikao hicho kinakuja kufuatia mashabiki wa Manchester United kuvamia nyumba ya Kaimu Mkurugenzi Ed Woodward kushinikiza aondoke madarakani.

Mashabiki hao walisikika wakisema kuwa “Tunaenda kukuua” huku wakilusha mawe kuelekea nyumba hiyo.

Nyumba haikuwa na mtu kwa muda huo. Baadhi ya mashabiki wamekuwa wakiimba nyimbo kama hizo za kushinikiza kuondoka kwa Mkurugenzi huyo katika michezo ya Burnley na Tranmere.

“Kufuatia matukio ya hivi karibuni, wawakilishi wa vilabu wameingia makubaliano ya kumfungia shabiki yeyote atakaye kiuka misingi ya soka kwa kutoa lugha chafu, lugha ya kibaguzi ama namna yoyote itakayo tafsiri na vilabu hivyo,” ilisema taarifa hiyo.

Awali ilikuwa kila timu inatoa adhabu kwa shabiki wake tu na adhabu hiyo ilikuwa haiingiliani na vilabu vingine, hii ina maanisha kuwa shabiki alikuwa akifungiwa na Manchester United alikuwa na uwezo wa kwenda kuangalia mechi za Liverpool,  Chelsea ama Arsenal bila shida lakini kwa sasa haitakuwepo tena kanuni hiyo.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends