Afrika Kusini yawaduwaza wenyeji Misri

Timu ya taifa ya Afrika ya Kusini imefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Kimataifa Afrika Afcon 2019 baada ya kuiduwaza timu mwenyeji Misri kwa goli 1-0 katika mtanange uliofanyika dimba la Alexandria Jumamosi usiku.
Hii inakuwa mara ya kwanza kwa taifa la Misri kuondolewa mapema kwenye mashindano ya Afcon ambayo taifa hilo limeandaa huku matokeo mabaya kuwai kutokea ilikuwa kumaliza nafasi ya tatu.
Ikiwa haina mastaa wengi wanaokipiga nje ya nchi yao, Afrika Kusini ilifanikiwa kupata goli kupitia kwa kiungo mshambuliaji wa Bidvets Lotch dakika za lala salama kipindi cha pili katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa kwa dakika zote 90.
Afrika Kusini ilikuwa haipewi nafasi ya kufanya vyema mbele ya Mapharao kutokana na kufanya vibaya kwenye hatua ya makundi ikipoteza mechi mbili na kushinda moja.
Matokeo hayo yana maanisha Afrika Kusini itacheza na Nigeria hatua ya robo fainali baada ya timu hiyo kuiondosha Cameroon kwa goli 3-2 mchezo wa mapema zaidi.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments