Afrika Yataka Kombe la Dunia Kila Baada ya miaka Miwili

25

Rais wa FIFA Gianni Infantino amesema Shirikisho la Kandanda barani Afrika CAF kupitia kwa Rais wa Shirikisho hilo bilioni Patrice Motsepe limethibitisha kuwa liko tayari kuunga mkono mpango wa kufanya fainali za Kombe la Dunia kufanyika kila baada ya miaka miwili tofauti na ilivyo sasa.

Kwa takribani miezi minne sasa Fifa imekuwa ikiendelea kupokea maoni ya wadau mbalimbali wa kabumbu juu ya mpango wa kufanyika kwa Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili, mpango ambao umekuwa ukipigiwa chapuo na moja ya Waalimu wenye heshima zao Fifa na duniani kote Arsene Wenger.

Infantino amesema licha ya uzuri wa mpango huo, mataifa ambayo yamekuwa yakinufaika na kufanyika kila baada ya miaka minne hayawezi kukubali lakini ni mpango mzuri kwa wachezaji na kiuchumi kwa mataifa husika.

Bara la Ulaya lenye uwakilishi wa timu za taifa 13 kwenye fainali za Kombe la Dunia ni moja ya mashirikisho ambayo hayaungi mkono hoja ya kufanyika kwa Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili, Shirikisho lingine ni lile la America Kusini (Conmebol).

“Kunapokuwa na mabadiliko lazima wajitokeza wale ambao hawapendi kuona hayo, na hawa ni wale wanaonufaika na ukale lakini kwa wale ambao hawanufaika nao watahitaji mabadiliko”, alisema Infantino.

“Hofu yao iko kwenye utawala wao, wakidhani kuwa likifanyika mara nyingi utawala unaweza kushuka, uzuri milango iko wazi, tunaendelea kupokea maoni zaidi”.

Afrika bado inawakilishwa na mataifa matano pekee kwenye fainali za Kombe la Dunia Qatar 2022 na kabla ya hapo, ingawa baada ya hizo fainali kutakuwa na nafasi nyingine moja, hata hivyo wanahitaji liwe linafanyika kila baada ya miaka miwili ili kutoa nafasi kwa mataifa mengi zaidi kushiriki lakini pia wachezaji wapate kulicheza zaidi ya mara tano, nne wazo ambalo hata Wenger amekuwa akilisimamia.

Author: Asifiwe Mbembela