Ajax kupumzika kabla ya kukutana na Tottenham

Wakuu wa kandanda la Uholanzi wamefuta mechi zote za ligi kuu ya nchini humo – Eredivise kabla ya Ajax kuumana na Tottenham katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ajax walitarajiwa kucheza dhidi ya De Graafschap Jumapili Aprili 28, kisha wasafiri kupambana na Spurs katika mkondo wa kwanza Jumanne Aprili 30.

Shirikisho la kandanda la Uholanzi – KNVB limesema uamuzi huo wa kufuta mechi za ligi kuu ulichukuliwa ili kuipa Ajax angalau siku mbili za kupumzika kati ya mechi hizo.

Limesema sio Ajax pekee itakayonufaika bali kandanda la Uholanzi kwa ujumla. KNVB ilikutana na wawakilishi wa vilabu siku ya Alhamisi kujadili mipango hiyo, na ikakiri kuwa wengi hawakufurahishwa na mabadiliko hayo.

Spurs watacheza dhidi ya Westham Jumamosi mchana Aprili 27. Hata hivyo, mchuano wa ligi dhidi ya Bournemouth Jumatatu usiku Mei 6 – siku mbili kabla ya mchuano wao wa marudiano wa nusu fainali unatatarajiwa kusogezwa na Ligi ya Premier.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends