Al Ahly kukwaruzana na Esperance fainali ya Champions League

Miamba wa Misri Al Ahly watalenga kuiendeleza rekodi yao kwa kutwaa taji la tisa la Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuweka miadi ya kucheza fainali na Esperance ya Tunisia. Ahly iliilaza Entente Setif ya Algeria kwa jumla ya mabao 3-2 kwenye nusu fainali ya mikondo miwili.

Ahly ilifuzu katika fainali licha ya kuchapwa 2-1 na Entente Setif katika mchuano wa mkondo wa pili wa nusu fainali yao nchini Algeria.

Esperance walipata ushindi wa 4-2 dhidi ya Primeiro Agosto ya Angola na hivyo kufuzu kwa jumla ya mabao 4-3. Esperance ilifungwa 1-0 katika mkondo wa kwanza.

Miamba hao wa Cairo Ahly watawaalika Esperance katika mkondo wa kwanza wa mechi ya fainali mnamo Novemba 2 huku mkondo wa marudio ukiwa Tunis siku saba baadaye.

Esperance walishinda Kombe hilo katika mwaka wa 1994 na 2011 na wakapoteza jumla ya mabao 3-2 dhidi ya Al Ahly katika fainali ya 2012.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends