Al Ahly yatwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Zamalek

Kikosi cha Al Ahly kimewaduwaza wapinzani wao wa jadi kutokea Jiji la Cairo Zamalek kwa kuwafunga goli 2-1 mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika Jana Ijumaa.

Goli la dakika za lala salama wakati mtanange ukionekana kuwa utaenda muda wa ziada la Mohamed Magdy akitokea nyuma kidogo ya lango la Zamalek lilihaikisha kuwa ubingwa unaenda kwa Al Ahly.

Bao la Magdy la dakika ya 88 lilikuwa la kufurahisha kwenye mechi ambayo ilikuwa inachezwa kama dabi zaidi kuliko fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Al Ahly walikuwa wa kwanza kujipatia bao kupitia kwa Amr El Soleya akipiga kichwa kikali pembezoni mwa mlingoti kabla ya nahodha wa kikosi cha Zamalek Shikabala kufanya mambo kuwa 1 – 1.

Mchezaji ghali wa kikosi cha Ahly Elshahat alikuwa kwenye nafasi ya kuipa ushindi timu yake baada ya mpira wake kugonga mtambaa wa panya ungwe ya kwanza kwenye mchezo uliokuwa bila mashabiki kutokana na changamoto ya Janga la virusi vya Corona.

Matokeo hayo yanaifanya Al Ahly kuendeleza rekodi bora barani Afrika katika kuchukua kombe la Ligi ya Mabingwa na sasa wanafikisha taji la tisa, wakati huo huo kocha wa Ahly Pitso Mosimane, anakuwa kocha wa tatu kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na vilabu viwili tofauti baada ya msimu Jana kubeba akiwa na Mamelodi Sundowns.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends