Aliyekuwa mkuu wa riadha Kenya apigwa marufuku miaka kumi
Kocha wa wanariadha wa timu ya taifa ya Kenya katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2016 mjini Rio de Janeiro amepigwa marufuku kwa miaka 10 kushiriki mchezo huo kwa kutoa taarifa ya mapema ya uchunguzi wa matumizi ya dawa zinazoimarisha misuli, doping, kwa wanariadha ili kujipatia fedha. Michael Rotich amepigwa marufuku , na kutozwa faini ya dola 5,000 leo, na bodi ya maadili ya shirika la vyama vya riadha duniani IAAF baada ya uchunguzi wa miaka mitatu.
Rotich alionekana katika kamera akitoa ombi hilo kwa mwandishi habari za uchunguzi kutoka gazeti la Sunday Times la nchini Uingereza, ambalo lilitoa vidio hiyo wakati wa michezo ya mjini Rio. Ujumbe wa Kenya katika michezo hiyo ulimrejesha Rotich nyumbani kutoka Brazil.