Ally Mayai, Tarimba wajitosa kuwania kiti cha Urais TFF

Leo Alhamis idadi ya wagombea wa kiti cha Urais wamefika saba kufuatia wagombea wawili wa nafasi hiyo kujitokeza katika Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu TFF kuchukua fomu za kushindania nafasi hiyo.

Wagombea hao wawili, ni nahodha na mchezaji wa zamani wa Yanga Ally Mayai Tembele pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kinondoni Abbas Tarimba ambapo fomu zote mbili zimechukuliwa na Mayai kwa kile kilichoelezwa kuwa Tarimba yuko kwenye majukumu ya kiserikali.

Akizungumza na Vyombo vya Habari Ally Mayai ambaye aliwania nafasi ya Urais uliopita uliompata Rais wa sasa Wallace Karia amesema ametumia demokrasia kuendelea kutafuta nafasi ya Urais akisema atasema mengi muda wa kampeni ukiwadia.

Wakati, Tarimba akizungumza na Shirika la Utangazaji TBC amesema amechukua fomu ingawa ugumu umekuwa kwenye upatikanaji wa Wadhamini watano kutoka vyama vya soka vya mikoa kwani wote wanaonekana kama wameshadhamini, akitaja kama ni figisu.

Wagombea wengine ambao wameshachukua fomu ni Rais anayetetea kiti chake Wallace Karia, Oscar Oscar, Deogratius Mutungi, na Zahor Mohammed Haji, Evans Mgeusa.

Zoezi la uchukuaji fomu linafikia tamati Juni 13, 2021 saa 10 jioni.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares