Alves ajiunga na klabu ya utotoni ya Sao Paulo

Mlinzi wa pembeni wa Brazil na nahodha wa kikosi hicho Dani Alves amejiunga na klabu ya utoto wake Sao Paulo katika uhamisho huru baada ya kucheza bara la Ulaya kwa miaka 17.

Alves, 36, msimu uliopita alikuwa anaitumikia klabu ya Paris St-Germain ambako alijiunga nayo akitokea Juventus. Baada ya PSG sasa amerejea nyumbani na kujiunga na Sao Paulo kwa kandarasi ya miaka mitatu hadi 2022. Itakuwa mara ya kwanza kucheza Brazil tangu 2002 alipokuwa na Bahia.

Alves anatajwa kama mchezaji aliyetwaa zaidi mataji na klabu kuliko wengine akiwa ameshinda mataji 40 katika muda wote huo kuanzia ngazi ya taifa na vilabu, amepita Barcelona, Juventus na PSG.

Rais wa Sao Paulo Carlos Augusto de Barros e Silva akizungumza baada ya usajili huo amesema, “Siku moja nilikuwa namwambia Daniel kuwa atakuja kucheza katika klabu hii, nimefurahi sana leo nimetimiza ahadi yangu kwa klabu hii”

Beki huyo alitajwa kuwa nahodha ya kikosi hicho kwenye mashindano ya Copa America baada ya aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho (Neymar Jr)  kuumia, ambapo pia alitajwa kama mchezaji bora wa mashindano hayo.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends