Ambundo, Ntibanzokiza Kuikosa Simba, Utovu wa Nidhamu Kambini

41

Yanga imewasimamisha wachezaji wake wawili kwa muda usiojulikana kutokana na kutoroka kambini (utovu wa nidhamu) wakati timu hiyo ikijiandaa na mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la TFF.

Yanga ambayo ni mabingwa mara 27 wa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara iko mkoani Shinyanga kujiandaa na mchezo wa ASFC dhidi ya Simba utakaochezwa uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza, Jumamosi ya Mei 28.

Wachezaji ambao wamesimamishwa ni kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi Saido Ntibanzokiza na winga wa kimataifa wa Tanzania Dickson Ambundo ambao wote kwa pamoja walitoroka kambini usiku wa Jumatatu baada ya mchezo wa Ligi dhidi ya Biashara United.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa timu hiyo Haji Manara amesema kocha Nasreddine Nabi ameamua kuwasisimamisha wachezaji hao na wakirudi Dar watafanya mazungumzo ili kujua nini ilikuwa tatizo.

Ntibanzokiza ni moja ya wachezaji wenye mchango mkubwa kwenye mafanikio msimu huu ambapo amesaidia kupatikana kwa magoli 11 wakati Ambundo amefunga magoli mawili kwenye mechi tatu zilizopita.

Author: Asifiwe Mbembela