Amiens wapinga kushushwa daraja ligi kuu ya Ufaransa, waingia mahakamani kwa hasira

48

Klabu ya Amiens iliyokuwa inashiriki ligi kuu ya Ufaransa Ligue 1 imesema imeanza rasmi hatua za kisheria za kutetea haki yao ya kucheza Ligue 1 baada ya kushushwa daraja kutokana na janga la virusi vya Corona.Tayari mabwenyenye Paris St-Germain wameshatwaa ubingwa huo huku vilabu viwili Amiens na Toulouse vikishushwa daraja kufuatia tamko la serikali ya Ufaransa kuufuta msimu wa michezo ya mwaka 2019-20.

Amiens walikuwa nafasi ya 19 katika msimamo wa Ligue 1, alama nne nyuma ya Nimes iliyokuwa juu yake na alama 10 dhidi ya timu ya mwisho kwenye msimamo wa ligi kuu ya Toulouse, michezo 10 pekee ilikuwa imesalia kutamatisha ligi hiyo.

Rais wa klabu Bernard Joannin amesema “hayakuwa maamuzi sahihi”.

Katika mkutano na Waandishi wa Habari Rais huyo amesema: “Tumebaini kuwa maamuzi yale hayakuwa na usawa kimichezo. Maamuzi ambayo sawa na adhabu kubwa kwetu. Sio haki.

“Tutajaribu kupambania hilo, kubadilishia isiyo haki kuwa haki kwa wanamichezo”.

Itakumbukwa mwezi Aprili, klabu ya Amiens iliandika na kupeleka maombi kwa Bodi ya ligi ya Ufaransa, na Shirikisho la nchi hiyo juu ya kuomba msimu wa 2020/2021 kuwe na timu 22 badala ya 20 kisha kwa msimu ujao ndio timu mbili zishuke daraja na ligi iendelee kama kawaida.

Tayari ligi mbalimbali ulimwenguni zimefuta ligi zao, hizi ni miongoni mwa hizo ligi ya Uholanzi ilishafutwa, Ubeligiji, Cameroon, Kenya, na ligi nyingine dunia zimeshafutwa kupisha maandalizi ya msimu ujao, kwa sababu ya Corona.

Author: Bruce Amani