Cameroon yatwaa ubingwa AFCON U17

Vijana wa Cameroon chini ya umri wa miaka 17 wametangazwa kuwa mabingwa wa kombe la mataifa Afrika kwa vijana wenye umri huo baada ya kuifunga timu ya taifa ya Guinea kwa penati baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare tasa ya 0-0, katika mchezo uliofanyika uwanja wa taifa DSM.

Guinea na Cameroon waliingia hatua ya fainali baada ya kushinda kwa matuta hatua ya nusu fainali wakati ambao Guinea iliitoa Nigeria huku Cameroon ikiiondosha Angola.

Katika mchezo wa hatua ya makundi zilipokutana timu hizi, Nigeria waliibuka na ushindi wa goli 2-0.

Licha ya kupoteza mchezo wa hatua ya makundi mapema, Guinea walionekana wameimarika sana kwa kushindana na Cameroon ambayo imejawa na vipaji lukuki.

Penati ya ushindi ya Cameroon  ilifungwa na Saidou Alioum ikifuta ndoto za kocha Mohammed Camara za kutwaa ubingwa wa kwanza wa historia kwa nchi ya Guinea U17.

Angola wamemaliza nafasi ya tatu baada ya kuifunga Nigeria goli 2-1 siku ya Jumamosi.

Nchi zote nne zimefuzu kwenda Brazil kwenye mashindano ya FIFA kombe la dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 baadae mwaka huu.

Author: Asifiwe Mbembela