Guinea Yapoteza Sifa Kuandaa Afcon 2025

Shirikisho la Kandanda barani Afrika Caf linatarajia kufungua fursa mpya ya kuandaa fainali za Kombe la Mataifa Bingwa Afrika Afcon 2025 kufuatia taifa la Guinea maandalizi yake kutoridhisha.

Inaelezwa kuwa taifa la Morocco liko tayari kwa ajili ya kuandaa fainali za mwaka 2025.

Taarifa za kuhamishwa kwa mashindano hayo zinakuja siku chache baada ya Rais wa CAF Patrice Motsepe kutembelea taifa la Guinea kwenye mji mkuu wa Conakry siku ya Ijumaa na kujionea mazingira kisha kutangaza kuwa maandalizi ya fainali hizo hayalizishi.

“Kombe la Afcon 2025 halitafanyika Guinea kama ambavyo ilipangwa awali kutokana na kutokuwepo kwa maandalizi mazuri (yanayojitosheleza)”, alisema Motsepe ambaye alikuwa na akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kikao na serikali ya mpito ya Guinea.

Moja ya sababu ya kushindwa kufanya maandalizi ya Afcon kwa Guinea licha ya kupewa taarifa mapema, mwaka 2014 ilikuwa mara ya kwanza kabla ya kuambiwa kuandaa fainali za 2023 kisha kuambiwa tena waandae za mwaka 2025 ni kukosa utulivu wa kisiasa.

Kwa sasa taifa la Guinea linaongozwa na serikali ya mpito ambayo iko chini ya Col Mamady Doumbouya ambaye alikuwa ni Mkuu wa majeshi nchini humo.

Author: Asifiwe Mbembela