Kinda Kibabage wa Tanzania ahamia ligi ya Morocco

Beki kisiki wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 na Klabu ya Mtibwa Sugar, Nickson Kibabage amesajiliwa rasmi na timu ya Difaa Hassan Jadidi inayoshiriki Ligi Kuu nchini Morocco Batola Pro kwa mkataba wa miaka minne (4).

Kibabage, 19, amejiunga na timu ya Difaa akitokea klabu ya Mtibwa Sugar ambayo ndio timu iliyomuibua kabla ya kufahamika. Hata hivyo angalau msimu 2018/2019 amepata nafasi ya kucheza timu ya wakubwa.

Mlinzi huyo ana uwezo wa kucheza nafasi za ulinzi wa pembeni namba tatu na beki ya kati amekabidhiwa jezi namba 43 mgongoni kutokana na umri wake kuwa mdogo.

Nickson Kibabage amekuwa katika kipindi cha mafanikio tangu kuibuliwa msimu wa 2017 ambapo alikuwa miongoni mwa vijana waliounda timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za AFCON za vijana Gabon na baadaya hapo akajiunga na Ngorongoro Heroes.

Anajiunga na Difaa, timu ambayo winga wa Kitanzania Saimon HappyGod Msuva anacheza akiwa kinara wa magoli katika timu hiyo, bila shaka Kibabage na umri wake atakuwa anapata mafunzo tosha kutoka kwa Msuva.

Nickson Kibabage anaungana na wachezaji wengine wawili waliounda kikosi kilichoshiriki fainali za Afcon kule Gabon kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania, wengine ni Yohanna Nkomola, na Ally Ng’anzi.

Soka la Tanzania limepiga hatua katika siku za hivi karibuni kutokana na idadi kubwa ya wachezaji kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi yao.

Author: Asifiwe Mbembela