Kipchoge abeba medali Olympiki Tokyo 2020

Mfukuza upepo wa kimataifa wa Kenya Eliud Kipchoge EGH amefanikiwa kutetea taji lake la medali ya Marathon na kuwa mwanariadha wa kwanza tangu mwaka 1980 kutwaa mfululizo Medali za Dhahabu za Marathoni kwenye Olimpiki na wa tatu tu kushinda mfululizo katika michezo hiyo.

Kipchoge mwenye umri wa miaka 36, akishindana na Mtanzania Alex Simbu na wanariadha wengine alifanikiwa kushinda kwa kutumia saa mbili, dakika nane na sekunde 38 pekee.

Akipewa hadhi ya mwana Marathon bora wa muda wote, mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 36 alimaliza dakika moja na sekunde 20 kabla ya Mholanzi Abdi Nageeye aliyechukua Fedha, wakati Mbelgiji Bashir Abdi alimshinda Mkenya mwingine, Lawrence Cherono na kuchukua Shaba.

Wengine katika 10 Bora ni Ayad Lamdassem wa Hispania aliyeshika nafasi ya tano, Suguru Osako wa Japan nafasi ya sita, Galen Rupp wa Marekani nafasi ya nane, Othmane El Goumri wa Morocco nafasi ya tisa na Koen Naert wa Ubelgiji nafasi ya 10.

Wanariadha wengine wa Tanzania walioshiriki Olimpiki ya Tokyo ni Gabriel Gerald Geay hakumaliza baada ya kuumia na Failuna Abdi Matanga ameshika nafasi ya 24 upande wa wanawake.

Yapata miaka 41 tangu Tanzania ilipotwaa kwa mara ya kwanza na ya mwisho Medali katika michezo ya Olimpiki – mwaka 1980 Jijini Moscow, Urusi kupitia kwa wanariadha Suleiman Nyambui Mujaya Mita 5000 na Filbert Bayi Sanka Mita 3000 wote wakishinda Fedha baada ya kumaliza nafasi ya pili.

Author: Bruce Amani