Korir na Rotich wawapa tabasamu Wakenya baada ya kushinda 1, 2 katika mita 800 Olimpiki

Mkenya Emmanuel Korir ameshinda leo taji la Olimpiki la mbio za mita 800 kwa wanaume huku mwenzake Ferguson Rotich akibeba nishani ya fedha. Korir alitumia muda wa dakika moja na sekunde 45.06 huku Rotich akimaliza katika muda wa dakika moja sekunde 45.23. Mpoland Patryk Dobek alibeba medali ya shaba.

Wakati huo huo, Peruth Chemutai amekuwa mwanamke wa kwanza Mganda kushinda medali ya dhahabu ya Olimpiki katika michezo yoyote baada ya kushinda leo mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa wanawake. Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 22 alitumia muda wa dakika 9 sekunde 1.45 na kumaliza sekunde tatu mbele ya Mmarekani Courtney Fredrichs aliyebeba fedha, huku Mkenya Hyvin Kiyeng akiridhika na shaba.

Author: Bruce Amani