Nigeria wawabwaga Afrika Kusini na kuhifadhi Kombe la AWCON

Nigeria ndio mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake 2018 – AWCON 2018 baada ya kuwashinda Afrika Kusini 4-3 kupitia penalty katika fainali iliyochezwa Jumamosi mjini Accra.

Mechi hiyo ilikamilika kwa sare ya 0-0 baada ya dakika 120, ambapo kipa wa Super Falcons Tochukwu Oluehi aliokoa mkwaju wa penalty kutoka kwa Linda Motlhalo wa Banyana Banyana.

Kiungo mwenye uzoefu Asisat Oshoala awali alikosa nafasi ya kuipa Nigeria ushindi katika muda wa kawaida baada ya kukosa penalty.

Mabinti hao wa Nigeria ambao waliingia mashindano ya mwaka huu wakiwa mabingwa watetezi, wanahifadhi udhibiti wao katika tamasha hilo, kwa kushinda kombe la tisa katika mashindano 11..

Nigeria na Afrika Kusini sasa wanajiandaa kucheza Kombe la Dunia mwaka ujao nchini Ufaransa ambapo wataungana na Cameroon ambao waliwalaza Mali na kuchukua nafasi ya tatu katika mashindano za AWCON 2018.

Author: Bruce Amani