Simba yatinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika

Ni mechi ambayo kwa vyovyote vile, walihitaji pointi tatu ili kujihakikishia nafasi ya robo fainali. Na hata msemaji wa klabu Haji Sunday Manara akasema kuwa itakuwa vita vya kufa au kupona.

Na baada ya dakika tisini, kelele za shangwe ndani ya uwanja wa Taifa Dar ziliweza kusikika hadi mitaa ya mbali jijini Dar es Salaam na kote Tanzania.

Mabingwa mara 19 wa Ligi kuu Tanzania bara Simba Sports Club wameandika historia ya kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuibuka na ushindi wa goli 2-1 dhidi ya AS Vita leo Jumamosi, mchezo ukifanyika dimba la Taifa, Dar es Salaam.

Kunako dakika ya 13 kipindi cha kwanza AS Vita walikuwa wanaongoza kwa goli moja kwa bila, goli likifungwa na Kazadi Kazengu na baadaye Simba wakasawazisha kupitia kwa Mohammed Hussein mnano dakika ya 36.

Mpaka kipenga cha mwamuzi kinalia kuashiria dakika 45 za kwanza zinamalizika matokeo yalikuwa 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Simba wakipigana kusaka bao la pili ili kupata nafasi ya kuingia hatua ya Robo Fainali. Huku kila Mwalimu akijaribu kufanya mabadiliko ya hapa na pale kukiimarisha kikosi kwa nafasi yake.

Jitihada za Simba kusaka bao zilifanikiwa baada ya kosakosa nyingi langoni kwa Vita ambapo Clatous Chama alifanikiwa kupachika bao la pili kwenye dakika ya 90 ya mchezo.

Bao la Chama limeweza kuipa Simba historia mpya ya kutinga hatua hiyo. Hii inakuwa mara ya pili kwa Chama kufunga goli muhimu kwa Simba baada ya lile la Makundi dhidi ya Nkana.

Msimamo wa kundi D hivi sasa unaonesha Al Ahly walioungana na Simba kufuzu wako nafasi ya kwanza wakiwa na alama 10 baada ya kuitandika JS Saoura mabao 3-0 leo.

Simba nao baada ya ushindi wa Jumamosi wamefanikiwa kumaliza wakiwa nafasi ya pili wakiwa na alama 9 huku Saoura wakiwa nafasi ya tatu na alama 8 pamoja na AS vita wakiwa wa nne na alama 7.

Mara ya mwisho Simba kufikia hatua hii ilikuwa mwaka 2003.
 
Je, Simba wamestahili nafasi hiyo? Tuachie maoni yako

Author: Asifiwe Mbembela