Weah arejea uwanjani dhidi ya Nigeria

Rais wa Liberia na mshindi wa zamani wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka Ulimwenguni George Weah alirejea tena uwanjani katika mchuano wa kimataifa mjini Monrovia, lakini timu yake ilipata kipigo cha mabao mawili kwa moja dhidi ya Nigeria. Mchuano huo ulikuja wiki chache tu kabla ya rais huyo kusherehekea miaka 52 ya kuzaliwa kwake.

Liberia iliandaa mchuano huo wa kirafiki ili kuistaafisha jezi nambari 14 iliyopewa umaarufu na Weah lakini mashabiki walipigwa na butwaa, miaka 16 baada ya Weah kucheza mechi yake ya mwisho ya kimataifa, kumuona mshambuliaji huyo akiiongoza timu yake kuingia uwanjani akiwa ameivaa jezi hiyo.

Weah alionyesha umahiri wake katika baadhi ya mashambulizi na akapigiwa makofi kutoka kwa mashabiki waliosimama kumuonyesha heshima wakati alipoondolewa uwanjani katika dakika ya 79. Mabao kutoka kwa Henry Onyekuru na Simeon Nwankwo yaliisaidia Nigeria kujiweka kifua mbele 2-0 kabla ya wenyeji kurejesha moja kupitia penalty ya Kpah Sherman

Katika taaluma yake ya muongo mmoja na nusu barani Ulaya alizichezea Monaco, Paris Saint-Germain na Marseille nchini Ufaransa, AC Milan ya Italia na Manchester City na Chelsea za England. Alishinda tuzo ya Mchezaji bora wa mwaka wa mwaka 1995, na pia Ballon d’Or mwaka huo huo, na ndiye mchezaji pekee wa Afrika kushinda tuzo hiyo mpaka sasa

Author: Bruce Amani