Amunike alitumia karata zake vizuri dhidi ya Cape Verde

114

Jioni ya Octoba 16 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kulizuka furaha kubwa sana na pengine naweza kusema ni furaha ambayo haijatokea kwa wapenzi wa soka hasa timu ya Taifa ya Tanzania tangu aondoke kocha mbrazil Marcio Maximo

Licha ya kukatishwa tamaa na matokeo ya ugenini ya kutandikwa magoli 3-0 dhidi ya Cape Verde siku 4 zilizopita lakini pia kandanda bovu waliloonyesha siku ya mchezo huo, Watanzania wengi hawakuwa na tumaini lolote juu ya mchezo wa marejeano dhidi ya Cape Verde

Kitu ambacho kilisababisha wapenzi wengi wa soka kutojitikeza uwanjani wengi wao wakisema hatuwezi kuja uwanjani kwa sababu hakutokua na jipya maana unagongwa tena na Cape Verde maana si kwa kiwango kile wakimaanisha mchezo wa kwanza ambao Tanzania ilipoteza ugenini

Lakini mpira ni mchezo wa ajabu maana mabadiliko ya kiuchezaji na mfumo ndani ya siku nne tu ilitosha kwa Taifa Stars kupindua matokeo na kuchomoza na ushindi wa magoli 2- 0 dhidi ya Cape Verde tena wakisakata kandanda safi zaidi ya matarajio ya wengi

Mwalimu Emmanuel Amunike bila shaka alisikia kilio na ushauri wa Watanzania na kwa haraka alifanya kazi na kuzaa matunda

Kwa matokeo ya ushindi wa magoli mawili dhidi ya wapinzani Cape Verde, ari na msukumo umerudi kwa mashabiki wa soka na sasa wapo tayari kwa mapambano

Watanzania walikua wanahitaji nini na walishauri nini? 

Katika mchezo wa kwanza dhidi ya Cape Verde, wadau wengi walikosoa mbinu Za mwalimu na pia upangaji wa kikosi ndicho kilichoigharimu Stars na kupata kipigo kile.

Hivyo Watanzania waliamini Kuwa kama mwalimu angewaheshimu na kuchukua tahadhari Kubwa dhidi ya Cape Verde basi tungeepuka na fedheha île kule Praia

Mwalimu Amunike aliwapanga Ramadhan Kessy, Gardiel Michael Mwantika na Aggrey Moris kitu kilichoonekana kupwaya katika ngome ya Stars wengi wakiamini beki Shomari Kapombe na Calvin Yondani wana ubora na kiwango cha kuanza katika timu hii

Kukosekana kwa beki Erasto Nyoni pia kulikua na tatizo kwa Stars kutokana na ubora na uzoefu wa beki huyo kiraka

Wadau hao walihitaji wachezaji hao wajumuishwe kikosini na hata timu ikifungwa basi hakutokua na lawama. Mwalimu amelifanyia kazi na hatimaye kuleta ushindi tena katika wakati muhimu

Katika mchezo huu wa marejeano tumeona timu imecheza vizuri na kwa uwelewano mkubwa katika Safu ya ulinzi Calvin Yondani, Shomari Kapombe na Erasto Nyoni wameleta uimara tofauti na mchezo iliyopita

Taifa Stars imeonyesha ukakamavu, upambanaji na kuna kila dalili ya kufanikiwa kupata nafasi moja wapo katika kundi L na  kuibuka kule Cameroon

Kutokana na matokeo haya, Stars imejongea hadi nafasi ya pili na sasa inapiga hesabu katika michezo miwili iliyosalia dhidi ya Lesotho ugenini na wa nyumbani dhidi ya Uganda na kama itachanga karata zake vema basi itapata nafasi moja Kati ya mbili za juu na kufuzu kwa AFCON 2019

Rai yangu kwa TFF na wadau wa soka ni kuwa mshikamano huu ulioonyeshwa usiishie hapa. Safari bado ni ndefu na ni ngumu kuelekea kwenye mafanikio

Author: Bruce Amani