Amunike asiwe kichaka cha kufichia mapungufu ya Taifa Stars

179

Kocha Emmanuel Amunike amekuwa kivuli cha kufichia udhaifu wa timu ya Tanzania “Taifa Stars”. Kila mmoja anamuona kama hafai, hana uwezo wa kukinoa kikosi cha Stars. Wengine wamekuwa wakithubutu kusema kama kwao Nigeria walimfukuza kazi ya ukocha ataweza kweli hapa.

Amunike amekuwa adui wa Watanzania wengi tangu awali licha ya kasi kuongezeka kwenye mchezo wa Lesotho. Matokeo ya Uganda yakawasahaulisha mashabiki na baadhi ya wadau wa soka nchini. Baada ya matokeo ya AFCON lawama zikaibuka kwa kiwango kikubwa zikimtaka asirudi Tanzania.

Je umejaribu kujiuliza kama Emmanuel Amunike anastahili lawama hizi?

Jibu binafsi ni hapana. Tanzania haihitaji kocha. Tanzania hata aje kocha gani bora, atashindwa. Kibaya zaidi, wengi wetu tunashindwa kutaja sababu kubwa ya kushindwa kufanya vizuri tunaishia kuwatupia lawama makocha, muda mwingine tukiwanyooshea vidole wachezaji. Hivi ni visababu vidogo vinavyopelekea sababu kubwa moja.

Labda kwa kumbukumbu tu tangu mwaka 2006 mpaka sasa Taifa Stars imefundishwa na waalimu 6 tofauti wote wametimuliwa kwa kigezo cha kushindwa. Inawezekana ni kweli lakini hakuna bora hata kidogo, utakachogundua tatizo halipo kwa makocha wala wachezaji.

Alipita Marcio Maximo akatoa mwanga, akaja Jan Poulsen, Kim Poulsen, Salum Madadi, Martin Nooij, Boniface Mkwasa na Salum Mayanga wote wakashindwa sasa Amunike.

Wamepita wachezaji wa kila kaliba na namna lakini wapi, tuko pale pale. Utarudi kukumbuka kuwa chanzo sio makocha wala wachezaji.

Kinachoiponza Tanzania sio kocha wala wachezaji ni kutokukubali kuwa soka ni sayansi yenye mifumo inayoonekana kabisa. Tanzania inajikita kubadilisha rangi ya nguo mwili unabaki kuwa ule ule.

Soka ni uwekezaji hasa katika zama hizi ambazo mpira ni ajira watu wanawekeza katika kuwaandaa wachezaji wadogo baada ya miaka michache wanavuna matunda mengi.

Itazame Senegal leo kwenye kikosi kilichoanza dhidi ya Tanzania hakuna mchezaji anayecheza soka la ndani. Watazame Ivory Coast wanacheza mchezo muhimu dhidi ya Bafana Bafana Afrika Kusini wanapata jeuri ya kumuweka Wilfred Zaha yule wa Crystal Palace nje.

Haitokei kama ajali bali ni uwekezaji wa mda mrefu uliopitia mifumo sahihi hivi sasa wana akina Zaha wengi, akina Sadio Mane wengi hata asipocheza huoni utofauti mkubwa wa kiuchezaji.

Siku ambayo viongozi wa TFF, Serikali na wadau wengine wa soka watakapogundua kuwa tatizo la soka sio makocha na wala sio wachezaji suluhu ya shida zinazopatikana sasa kama kufananishwa na kichwa cha mwendawazimu zitamalizika kabisa kwa sababu sio uchawi.

Mifumo sahihi ya uendeshwaji wa michuano ya ndani kama ligi, mashindano ya FA, michezo ya vijana kwa umri wote, sio tu kufanyika kwa michezo bali kufuata taratibu na kuacha janja janja ambazo zimefanyika muda mrefu na kuleta matokeo haya.

Binafsi licha ya changamoto hizi naona mwanga kwa siku za usoni hasa kupitia ligi za vijana ambazo zinafanyika pamoja na kwamba mwendelezo wa vipaji umekuwa hafifu na kuanza kila siku.

Author: Bruce Amani