Arsenal yaanza kibabe EPL kwa kuvuna pointi tatu dhidi ya Fulham

Mabingwa wa Ngao ya Jamii Arsenal wameanza kwa ushindi mnono wa goli 3-0 dhidi ya Fulham katika mchezo wa ufunguzi wa pazia la Ligi Kuu nchini England mtanange uliopigwa dimba la Craven Cottage leo Jumamosi.

Kikosi cha Arsenal kilicho chini ya kocha Mikel Arteta kilianza na maingizo mapya ambayo ni Willian winga kutokea Chelsea na mlinzi wa Kibrazil Gabriel wa Lille.

Willian amehusika kwenye bao zote tatu baada ya kutoa asisti kwa mabao ya Alexandre Lacazette na Aubameyang.

Alexandre Lacazette alikuwa wa kwanza kufunga goli, bao lililoandikisha rekodi kwa strika huyo kwa kufunga goli katika kila mechi ya ufunguzi wa EPL baada ya msimu uliopita kufunga dhidi ya Leicester City.

Wakati huo huo Gabriel alihusika katika goli la pili akimalizia kona ya Willian kabla ya nahodha wa kikosi hicho Pierre Emerick Aubameyang kufunga bao la mwisho kwenye ushindi mnono ikiwa ni mechi ya kwanza.

Akizungumza baada ya mchezo Kocha Arteta amekiri kushangazwa na kiwango kizuri cha Gabriel katika mechi yake ya kwanza tangu Ligue 1 iliposimamishwa mwezi Machi na baadae kufutwa kabisa.

Fulham walikuwa hovyo, hata nafasi chache walizozitengeneza walishindwa kuzitumia vizuri kupitia kwa mfungaji bora ndani ya klabu hiyo Aleksandar Mitrovic ingawa juhudi zao zilikuwa zinakwamishwa na Bern Leno.

Kwingineko klabu ya Crystal Palace imeibuka kidedea dhidi ya Southampton kwenye mechi ya ufunguzi pia kwa ushindi wa goli 1-0.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends