Arsenal yaendeleza ubabe kwenye Ngao ya Jamii, yaiduwaza Liverpool

343

Arsenal imeiduwaza Liverpool kwa kushinda mtanange kwa njia ya penati baada ya sare ya goli 1-1 kwenye mchezo wa Kombe la Ngao ya Jamii uliopigwa dimba la Wembley leo Jumamosi Agosti 29.

Alikuwa ni mshambuliaji wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang ambaye aliandikisha goli la kwanza akimalizia pasi ya kinda wa timu hiyo Bukayo Saka kabla ya bao hilo kusawazishwa na Takumi Minamimo kunako ungwe ya pili ya mchezo.

Liverpool ambao ni mabingwa wa EPL kwa msimu 2019/20 walijikuta wakipoteza uwezo wao wa msimu uliopita baada ya Arsenal kuonyesha kiwango kizuri hasa eneo la ulinzi ambalo David Luiz na Holding walitengeneza muunganiko bora.

Licha ya piga nikupige, mpaka dakika za mwamuzi zinakamilika Liverpool 1-1 Arsenal. Ikafika wakati wa matuta ambapo mchezaji pekee aliyekosa tuta ni kinda Rhian Brewster baada ya mpira wake kugonga mtambaa wa panya.

Inakuwa mara ya pili mfululizo Liverpool wanapoteza kwa penati baada ya kutokea hivyo kwa mwaka 2019 walipocheza dhidi ya Manchester City, wakati Arsenal wanafanikiwa kutwaa taji la 16 la Ngao ya Jamii.

Waliotupia nyavuni matuta ya Arsenal ni Nelson, David Luiz, Cedric Soares, Maitland-Niles, na Aubameyang alitupia penati ya mwisho na ya ushindi kwa Liverpool.

Wakati Liverpool waliofunga ni Mohammed Salah, Takumi Minamimo, Fabinho, Curtuis Jones na penati iliyokosa kuingia nyavuni ni yake Brewster.

Author: Asifiwe Mbembela