Arsenal yakaribia kunasa saini ya winga wa Kibrazil Willian kutoka Chelsea

Arsenal inakaribia kukamilisha usajili wa winga wa Chelsea na Brazil Willian. Winga huyo atakuwa nje ya mkataba wake wa sasa baada ya kumalizika kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Ulaya mwishoni mwa mwezi wa nane.

Willian, 31, na klabu ya Chelsea hawajafikia makubaliano yoyote huku kukiwa na tetesi kubwa ambazo zinamhusisha staa huyo kutua ndani ya Washika Mtutu wa London Arsenal na kuungana na aliyekuwa mchezaji mweza David Luiz.

Chelsea walimpa ofa ya mkataba wa miaka miwili Willian lakini anaonekana kutokuwa tayari kuingia kwenye mkataba mwingine The Blues, badala yake anaelekea kukubali mkataba wa miaka mitatu wa kujiunga na Arsenal iliyo chini ya kocha Mikel Arteta.

Willian alikosa mechi iliyoisha kwa kipigo kwa Chelsea fainali ya Kombe la FA dhidi ya Arsenal wikendi iliyopita ambapo kuna wasiwasi pia atakosa mechi ijayo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayerm Munich raundi ya pili baada ya awali kukubali kichago cha goli 3-0 dimba la nyumbani.

Willian alisajiliwa na Chelsea mwaka 2013 akitokea timu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi na tayari amecheza mechi 339 akiwa na The Blues, ameshinda tuzo tano kubwa ikiwemo mara mbili ligi kuu, Europa ligi na kushinda tuzo ya mchezaji bora wa klabu wa msimu mara mara mbili.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends