Atletico nje ya Copa del Rey lakini Real yafuzu licha ya kipigo

122

Klabu ya Atletico Madrid imeondoshwa katika mashindano ya Copa Del Rey dhidi ya kibonde Ginoa baada ya sare ya goli 3-3 huku wageni wakifanikiwa kusonga mbele kwa faida ya goli la ugenini.

Atletico ilianza vyema katika kipindi cha kwanza baada ya Nikola Kalinic kufunga goli la mapema.

Baadae Valery Fernandez na Cristhian Stuani kwa upande wa Ginoa walifunga goli moja kila mmoja na kufanya ubao kusomeka 2-1 kabla ya Angel Corea kusawazisha goli hilo.

Bingwa wa kombe la Dunia nchini Urusi mwaka 2018 Antoine Griezmann alifunga goli ambalo lilionekana kama kuisogeza Madrid katika hatua ya nane bora lakini Sedou Doumbia alifuta ndoto za Atletico baada ya kufunga goli upande wa Ginoa.

Katika matokeo mengine ya michuano hiyo Real Madrid ilibamizwa na Leganes goli 1-0 lakini ikasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa goli 3-1.

Mshambuliaji wa Kidachi Martin Braithwaite, 27, alifunga goli kwa upande wa Leganes kupitia mpira uliotemwa na kipa Navas dakika chache baada ya mpira wa kichwa kugonga mtambaa wa pacha.

Katika hatua nyingine Sevilla ambayo ipo nafasi ya tatu kwenye La Liga imeingia hatua ya nane bora baada  kuifumua Athletic Bilbao kwa jumla ya goli 3-2, licha mchezo wa mkondo wa pili kupoteza kwa 1-0. Gorka Guruzeta ndiye aliyepeleka kilio kwa Sevilla ingawa halikuisaidia timu hiyo kusonga mbele.

 

Author: Bruce Amani