Atletico yaichinja Barcelona nusu fainali ya Super Cup

Goli la dakika za jioni lililofungwa na Angel Correa liliipa ushindi Atletico Madrid wa goli 3-2 dhidi ya Barcelona na kuiondosha rasmi Barca kwenye michuano ya Super Cup iliyofanyika nchini Saudi Arabia likiwa ni kombe linalozikutanisha timu bora nne kutoka Copa Del Rey na La Liga.

Koke alikuwa wa kwanza kuandika goli upande wa Madrid kabla ya Lionel Messi kusawazisha kwa Barca likiwa goli lake la kwanza mwaka 2020, mpira wa kichwa wa Antonio Griezmann uliipa uongozi Barcelona mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Mshambuliajiwa zamani wa Juventus ya Italia, Chelsea na Real Madrid Alvaro Morata aliweka mtanange kuwa sawa kwa penati na kufanya matokeo kuwa 2-2 kabla ya shuti kali ya Correa kuamua mtanange wa Super Cup na kuiondosha Barca.

Matokeo hayo yanaifanya Atletico Madrid kuungana na Real Madrid kucheza fainali siku ya Jumapili wakati Wanacatalunya Barcelona na Valencia wakiaga mashindano hayo rasmi.

Tofauti na misimu mingine msimu huu mashindano hayo yalikuwa yanahusisha timu nne, timu mbili za juu kwenye msimamo wa La Liga msimu uliopita na timu iliyofika fainali ya Copa Del Rey wakati hapo awali timu mbili tu zilikuwa zikichuana.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends