Azam FC yaweka historia katika Kombe la FA

Mabingwa wa Kombe la Kagame Azam FC wameandika rekodi ya kutwaa Kombe la Shirikisho la soka Tanzania mara ya pili tangu kurejea kwa kombe hilo. Azam imepata ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Lipuli FC katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.

Goli pekee la juhudi binafsi la Obrey Chirwa mnamo dakika ya 64 ya kipindi cha pili limeipa Azam matokeo hayo na kuiwezesha kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) msimu ujao.

Mechi hiyo ambayo imekuwa ya kwanza kwa fainali ya FA kupigwa mkoani Lindi, imeshuhudiwa na watazamaji wengi ambao walijitokeza kwenye Uwanja wa Ilulu, na hii ni kutokana na ugeni wa timu hizo mbili mjini humo.

Matokeo hayo yanaifanya Azam kutinga kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza kupitia mashindano haya ya ASFC.

Aidha, Azam wameingia fainali kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwa michuano hii baada ya kushinda msimu wa 2014/2015 na kupoteza msimu wa 2015/16 dhidi ya Yanga kwa mabao 3-1, mechi ikichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ikumbukwe Lipuli walifanikiwa kutinga hatua ya fainali kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga huko uwanja wa Samora Mkoani Iringa na Azam wakiifunga KMC bao 1-0, mechi ikichezwa Chamanzi Complex.

Ukiachana na Azam kuwa bingwa hii leo, taji hilo lilichukuliwa na Mtibwa Sugar msimu wa 2017/2018 ambayo ilitwaa kwa kucharaza Singida United kwa jumla ya mabao 3-2, mechi ikichezwa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Azam ilifanikiwa kutengeneza historia ya kuwa timu ya kwanza kushinda taji la FA mara mbili 2014/2015, 2018/2019 huku fainali ya 2015/2016 ikipoteza. Timu zote zimelitwaa Kombe hilo mara moja.

Author: Bruce Amani