Azam hoi mbele ya Wazimbabwe Kombe la Shirikisho

Kikosi cha Azam kimepoteza mchezo wa kwanza hatua ya kwanza kwenye Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Triangle United kutoka Zimbabwe kwa goli 1-0 mchezo uliofanyika Jumapili Sept 15 katika dimba la Azam Complex nje kidogo ya Dsm.
Matokeo ya kupoteza kwa Azam yanakuja kipindi ambacho matajiri hao wamekuwa wakionyesha kiwango bora na kutopoteza mchezo wa kimataifa katika dimba la nyumbani Azam Complex tangu mwaka 2008.
Matokeo hayo yanaongeza ugumu wa wawakilishi wa Tanzania kufanya vizuri kama msimu uliopita kuendeleza nafasi ilizozipata msimu huo kwa sababu, Yanga pia ilishindwa kutumia faida ya uwanja wa nyumbani.
Goli pekee la wapinzani wa Azam FC, Triangel United ya Zimbabwe lilifungwa dakika ya 34 na nahodha Ralph Kawondera kutokana na uzembe wa safu ya ulinzi wa Azam FC.
Licha ya Azam FC kupewa sapoti kubwa na mashabiki waliojitokeza uwanja wa Azam Complex hayakuzaa matunda kwani safu ya ulinzi ya Triangle United ilikuwa ngumu na ikajilinda kwa takribani dakika 90 wakicheza kwa michezo ya kushitukiza.
Sasa Azam FC ina kazi nzito ya kwenda kutafuta matokeo ugenini kwenye mchezo wa marudiano unaoatarajiwa kuchezwa kati ya Septemba 27-29 nchini Zimbabwe.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends