Azam, KMC, JKT zavunja kambi za mazoezi hofu ya COVID-19

Klabu za Azam FC, JKT Tanzania, na KMC zimevunja rasmi kambi za mazoezi na kuwaruhusu wachezaji wote kurudi makwao.

Taarifa rasmi zilizotolewa na vilabu hivyo kwa wakati tofauti zimethibitisha kuwa zinavunja kambi kwa muda wa siku thelathini kuanzia jana Jumatano.Hatua hiyo inakuja kufuatia tamko la Serikali hapo jana, Machi 17, 2020, kupitia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Katika tamko lake, Majaliwa alitangaza kusimamisha kwa mwezi mmoja shughuli kadhaa zinazosababisha msongamano wa watu, ikiwemo mechi za mpira wa miguu, kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona, ambavyo vimeingia nchini.

Kutokana na hilo, kambi zote, kuanzia ile ya vijana chini ya miaka 17, vijana chini ya miaka 20 na timu ya wakubwa, zimevunjwa mara moja.

Kambi hizo zitarejea tena Aprili 17, 2020, ambao ni mwezi mmoja kamili kama alivyoagiza Waziri Mkuu. Azam FC, JKT Tanzania na KMC inaungana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Shirika la Afya Duniani, WHO, katika kutoa wito kwa wananchi kufuata maelekezo ya kitaalamu ili kujilinda na maambukizi ya maradhi haya hatari.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends