Azam, Simba zaiwachia kibarua Yanga

102

“HAKUNA KUREMBA” Unaweza kutumia msemo huo kwa sasa katika mbio za taji la ligi kuu ya Tanzania (TPL) Msimu wa 2018/2019 kwa Mafarasi watatu: Yanga, Simba na Azam ambao dhahiri shahiri wanaonyesha mmoja kati ya hao  anaweza akabeba taji hilo.

Wikiendi hii kulikua na michezo mingi sana ya ligi kuu lakini mashabiki wengi wanaziangalia mbio za farasi hawa nani atajikwaa na nani atakua na kasi zaidi ya mwenzake kuelekea katika taji

Azam FC ambao mpaka sasa hawajadondosha pointi tatu katika mchezo mmoja wamezidi kujikita kileleni baada ya kuchomoza na ushindi wa goli 1 – 0 ugenini dhidi ya Singida United katika uwanja wa Namfua uliko Kanda ya kati Mkoani Singida kwa goli pekee la mshambuliaji wa Kizimbabwe Donald Ndombo Ngoma.

Ngoma aliyesajiliwa toka Yanga kwa muda mrefu alikosekana dimbani kutokana na kusumbuliwa na maumivu, lakini kwa sasa ameanza kurejea makali yake na amekua anaifungia Azam FC magoli muhimu hivyo kuwa na matarajio ya kufanya vyema msimu huu, tofauti na ilivyofikiriwa na wengi kabla ligi kuanza

Hilo ni joli la pili kwa mshambuliaji huyo na Kocha Mkuu wa Azam, Hans Pluijm amesema amempa Ngoma kazi mbili uwanjani akishindwa kufanya moja ni lazima afanye ya pili ili kuisaidia timu kupata matokeo.

Azam sasa inafikisha pointi 27 mara baada ya kushuka dimbani mara 11 ikishinda michezo nane na kwenda sare michezo mitatu ikifunga magoli 14 na kuruhusu nyavu zake kutikisika mara mbili tu, unaweza kusema Azam ndio timu yenye rekodi bora mpaka sasa katika ligi kuu msimu huu

Wekundu wa Msimbazi wawaangamiza Ruvu

Wekundu wa Msimbazi Simba jana wamepata ushindi mpana wa magoli 5 – 0 dhidi ya Ruvu Shooting na kudhihirisha ubora wake hasa katika safu ya ushambuliaji huku mkali Emanuel Okwi akifunga magoli 3 hat trick na magoli mengine yakifungwa na Mkongwe Meddie Kagere na Adam Salamaba na kuzima kabisa tambo za Masau Bwire

Simba wanaonekana kurejea katika ubora wao baada ya kusuasua kidogo kwa kudondosha pointi saba katika michezo 10 waliocheza: pointi tatu walidondosha dhidi ya Mbao FC kule Kirumba Mwanza, pointi mbili wakidondosha katika uwanja wa Nangwanda Sijaona Mkoani Mtwara dhidi ya Ndanda na nyingine mbili walidondosha katika mchezo dhidi ya watani wao wa jadi  Yanga katika dimba la Taifa.

Kwa ushindi huo dhidi ya Ruvu Shooting walioupata Oktoba 28 katika uwanja wa Taifa wanafikisha pointi 23 katika nafasi ya pili baada ya kushuka dimbani mara 10

Kibarua sasa ni kwa Yanga

Young Africans ambao hawajapoteza mchezo katika ligi kuu msimu huu wameachiwa kibarua na timu za Azam na Simba sababu tayari wao wameshaibuka na ushindi katika michezo yao ya mwisho kimbembe ni kwa Yanga ambao Oktoba 30 watashuka katika dimba la Taifa kuwakabili Lipuli ya Iringa wana Paluengo.

Yanga imesalia nafasi ya tatu na alama 19 na michezo mitatu mkononi  na ina kazi ya kufanya vema katika mchezo huo ili ijizatiti katika nafasi za juu ambazo Simba pamoja na Azam wamekomaa kileleni

Kwa ujumla unaweza kusema ligi kuu msimu huu ina ladha yake kwa mafarasi watatu kukimbizana kileleni kila mmoja wao akiwa na uhakika wa kumaliza kinara wa ligi hiyo na kupata nafasi ya kuwakilisha Taifa katika michuano ya ligi ya Mabingwa barani Afrika kwa msimu husika.

Author: Bruce Amani