Azam yaduwazwa na KMC kwa kalambishwa 1 – 0

Kikosi cha Kinondoni Municipal Council – KMC kimewaduwaza vinara wa Ligi Kuu nchini Tanzania klabu ya Azam FC baada ya kuitandika goli 1-0 katika mchezo uliopigwa dimba la Uhuru Jijini Dar es Salaam leo Jumamosi.

Azam wakiwa wanaongoza ligi walikutana na mbinu bora za Kaimu Kocha Simkoko na Habibu Kondo wa KMC na kuzimwa kabisa juhudi za upatikanaji wa goli.

Bao pekee la KMC lilifungwa na Relliats Lusajo mshambuliaji wa zamani wa Namungo dakika ya 57 na kufanya Azam FC wakwame kwa mara ya kwanza wakiwa Dar kwa kuwa ule mchezo wa kwanza walipoteza wakiwa uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Matokeo hayo yanaifanya Azam kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa VPL ikiwa na alama zao 25 baada ya kucheza mechi 10, mchezo wa leo unakuwa wa pili kupoteza alama tatu baada ya ule wa Mtibwa Sugar.

KWINGINEKO

Wakati Azam FC ikipoteza kwa kufungwa bao 1-0 Uwanja wa Uhuru, JKT Tanzania ikiwa nyumbani, Uwanja wa Jamhuri Dodoma imefungwa mabao 2-0 dhidi ya Gwambina.

Mabao ya Gwambina yamefungwa na Paul Nonga dakika ya 84 likiwa ni bao lake la kwanza ndani ya ligi kwa msimu huu wa 2020/21 na Meshack Abraham dakika ya 72 ambaye anafikisha bao lake la tano.

Author: Asifiwe Mbembela