Azam yarudisha uwanja wa taifa mechi ya Simba, Yanga

Mabingwa wa Afrika Mashariki na kati Azam FC kupitia uongozi wa timu hiyo umeandika barua ya kuomba kurejesha mechi zao dhidi ya Simba SC na Yanga SC za ligi kuu Tanzania bara (TPL) msimu huu kufanyika katika uwanja Taifa Jijini Dar es salaam.

Sababu kubwa kwao ni kushindwa kuvumilia changamoto za mashabiki kwenye uwanja wa Azam Chamazi Complex katika michezo dhidi ya timu hizo mbili.

Ikumbukwe ni msimu wa 2017/2018  umepita tangu klabu ya Azam kutangaza kwamba haitautumia uwanja wa taifa katika michezo miwili ya Simba na Yanga kutokana na kuwa na uwanja wao,

Lakini leo kupitia kwa msemaji mkuu wa klabu hiyo Jaffar Idd sasa wapo tayari michezo yote miwili kupigwa katika dimba la Benjamin Mkapa ili kupunguza kero kwa mashabiki.

Kauli ya Idd inakuja baada ya Shirikisho la Soka TFF na Bodi ya ligi mwanzoni mwa msimu huu kutangaza kuwa kila mwenyeji wa mechi katika uwanja husika atachukua mapato yote tofauti na ilivyokuwa awali.

Katika kipindi hiki Azam wanatazamia kuwa na mapato mengi kutokana na watazamaji wanaoingia uwanjani katika mechi hizi.

Msimu uliopita Simba na Yanga zilicheza na Azam katika uwanja wa Chamazi bila shida ingawa baadhi ya mashabiki huwa wanakosa fursa ya kuangalia mchezo huo  kwa sababu ya udogo wa uwanja huo.

Barua yao imeandikwa rasmi siku ya Alhamis Novemba 15, 2018 na kupitishwa  na Mtendaji mkuu wa Azam FC Abdulkarim Mohemed Damian ‘Popat’

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends