Azam yavuliwa rasmi ubingwa wa Mapinduzi

49

Simba inatinga rasmi fainali ya Kombe la Mapinduzi kwa ushindi wa penalti 3 – 2 walizopata dhidi ya Azam FC baada ya mchezo kumalizika kwa sare tasa, mtanange uliopigwa dimba la Amani Zanzibar leo Ijumaa.

Simba wakitawala mchezo kwa kiasi kikubwa walishindwa kuifungua safu ya ulinzi ya Azam, mabadiliko pia hayakuleta tija kwenye vikosi vya timu zote mbili. Majaribio kadhaa kutoka kwa Fransis Kahata, Meddie Kagere na Ibrahim Ajib hayakufua dafu, hata yale ya Azam kutoka kwa Obrey Chirwa, Chilunda Shaban yakiwa chakula kwa Kakolanya.

Kipenga cha mwamuzi kilipigwa kuashiria tamati ya dakika 90 na hivyo hatua ya matuta akifuata.

Simba penati zake zilipigwa na Erasto Nyoni, Jonas Mkude, John Bocco wakati ile ya Shiboub na Kagere zikiokolewa na mlinda mlango Razack Abarola.

Azam penati zilipigwa na  Yakub Mohammed, Bruce Kangwa ambapo Ngoma Donald, Idd Kipwagille na Abarola zikishindwa kugusa nyavu za Beno Kakolanya.

Tamati ya mchezo huo ina toa picha kwamba Simba itakutana na Mtibwa Sugar hatua ya fainali tarehe 13 huku Azam Fc wakivuliwa rasmi ubingwa wa michuano hiyo.

Mara ya mwisho Simba kukutana na Mtibwa fainali ya michuano hiyo ilikuwa mwaka 2015 ambapo mchezo uliisha kwa sare ya tasa kabla ya penati kuamua pambano hilo

Author: Bruce Amani