Baada ya Simba, Yanga nayo yajiondoa Kombe la CECAFA

Klabu ya Yanga kutoka Dar es Salaam haitoshiriki mashindano ya Klabu Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) iliyopangwa kuanza kutimua vumbi Julai mwaka huu nchini Rwanda.

Taarifa ya kutoshiriki kwa Yanga imekuja kipindi ambacho hakizidi hata wiki moja tangu Katibu Mkuu wa CECAFA Nicolas Musonye aiandikie Yanga barua ya kuiomba kushiriki michuano hiyo baada ya msimu wa mwaka jana 2018 Yanga pia kususia kushiriki.

Kupitia ukurasa rasmi wa Yanga, taarifa ya kutoshiriki iliwekwa ikibainisha sababu mbalimbali za kutoweza kushiriki mashindano hayo.

Moja ya sababu ni asilimia kubwa ya kikosi chake kumaliza mikataba hivyo sio wachezaji wao hata wale wanaosajiliwa bado hawajakamilisha taratibu zote za kujiunga na timu hiyo. Pili ni kocha wa timu hiyo Mwinyi Zahera kuwa na majukumu mengine ya timu ya taifa ya Congo kwenye mashindano ya AFCON.

Mbali na sababu hiyo Yanga imesema imepanga kuanza maandalizi ya msimu ujao mapema ili kujiweka sawa na Ligi ya mabingwa, Mapinduzi, SportPesa na Ligi kuu.

Yanga inakuwa timu ya pili kujiondoa baada ya Simba nayo kujiondoa zote timu za Dar es Salaam.

Mashindano ya Kombe la Kagame yana utaratibu wa kufanyika kila mwaka kwa kuhusisha timu za Afrika Mashariki, yakidhaminiwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame ambapo jina la kombe hilo limetoka kwake.

Bingwa mtetezi wa taji hili ni Azam lakini miaka ya hivi karibuni michuano hiyo imekosa mvuto na ushindani huku ukosefu wa uongozi imara na upungufu wa ushindani kwa timu husika ukiwa chanzo kikubwa ya kupotea kwa mvuto wa michuano hiyo iliyokuwa na umuhimu mkubwa katika kuunganisha mataifa husika.

Author: Asifiwe Mbembela