Bale ajiondoa katika ziara ya Real Madrid Ujerumani

47

Gareth Bale amekumbwa na kadhia nyingine ya kuachwa nje ya kikosi cha Real Madrid kilichosafiri kuelekea Munich kwa ajili ya michezo mitatu ambapo Jumanne Julai 30 itacheza na Tottenham, ikiwa ni siku moja baada ya dili la kujiunga na China kuporomoka.

Imefahamika kwamba Bale ameachwa ili kujiweka sawa kiakili baada ya kuwa kwenye mgogoro na kocha Zinedine Zidane kutaka kuuzwa kabla ya Rais wa Madrid Florentino Perez kuzuia kujiunga na Jiangsu Suning.

Wiki iliyopita kocha Zidane alikaririwa akisema “Gareth yuko mbioni kuondoka klabuni”.

Madrid ambayo ni Mabingwa mara 33 wa La Liga watacheza na Tottenham Jumanne, ikifuatiwa na Bayern Munich na kumalizia na Fenerbahce katika michezo mitatu ya kujiandaa ya msimu mpya wa kimashindano.

Bale alijiunga na Madrid mwaka 2013 kwa dau la pauni milioni 85, ambapo msimu uliopita alicheza mechi 42 huku akizomewa na mashabiki wa timu hiyo.

Kocha Zinedane alionyesha nia ya kutomhitaji tangu kurejea kwae klabuni, ambapo katazo la kutouzwa limefikia baada ya Rais wa Madrid Florentino Perez kuhitaji hela kubwa ya uhamisho wa staa huyo.

Author: Bruce Amani