Barbara Anaondoka Simba, Lakini…

263

Siyo habari mpya tena kwamba Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzales, ataondoka ndani ya klabu hiyo Simba siku 20 zijazo. Lipo wazi. Ni baada ya yeye mwenyewe kuweka wazi uamuzi wa kujiuzulu nafasi yake hiyo, huku akitoa sababu kuu mbili nzito za kufikia uamuzi huo.

Barbara ambaye alichukua kijiti cha aliyekuwa mtangulizi wake Senzo Mbatha mnamo Novemba 17, 2022 katika kipindi hicho alikuwa mwenye mafanikio binafsi (kiutendaji) hali kadhalika timu imepata mafanikio.

Moja ya mafanikio binafsi ni nguvu ya ushawishi, hapa hauitaji kuwa na elimu yenye mihuri na saini kutoka kwenye taasisi, mashirika au wizara ya elimu kutambua hilo.

Aliweza kushawishi makampuni kuwekeza Simba, Wekundu wa Msimbazi waliweza kuingia mikataba kila baada ya kipindi fulani tena mikataba iliyonona, mathalani mkataba na kampuni ya kubashiri ya M.Bet.

Barbara, kijana anayetajwa na wikipidia kuwa ana miaka 32 kwenye andiko lake la kuutaarifu umma kuondoka lina sababu kuu mbili kutoa nafasi kwa Bodi Mpya ya Wakurugenzi itakayochaguliwa kwenye uchaguzi ujao kuchagua CEO mpya atakayeendana na dira yao. Pili kujipa nafasi ya kutimiza ndoto na fursa nyingine kwingineko.

Sababu hizi bila shaka zinaukakasi kiasi, iweje mtu ambaye amefanya makubwa kiasi hiki kuondoka na kuchaguliwa mtu mwingine zaidi kwenye kauli ya “atakayeendana na dira yao” pili hata kwenye sababu ya kutimiza mambo binafsi inaweza kuwa kichaka cha kujificha katika haya yanayoendelea kusemwa semwa chini ya kapeti.

Author: Asifiwe Mbembela