Barca yachapwa 2-1 nyumbani na Granada, furaha kwa wapinzani

Kikosi cha kocha Ronald Koeman Barcelona kumepoteza nafasi ya kwenda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu nchini Hispania La Liga baada ya kukubali kipigo cha goli 2-1 kutoka kwa Granada mchezo uliopigwa dimba la Camp Nou Leo Alhamis.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina Lionel Messi aliipa uongozi Barca akimalizia mpira wa winga wa kimataifa wa Ufaransa Antoine Griezmann.

Barcelona walikosa nafasi nyingi za wazi kabla ya Darwin Machis kufunga goli la kusawazisha kipindi cha kwanza.

Mchezaji wa akiba Jorge Molina aliingia na kutoka na alama tatu muhimu baada ya kufunga goli la ushindi kwa Granada ambao wanahitaji kushiriki michuano ya Ulaya kwa msimu ujao 2021/22.

Ushindi kwa Barcelona ungeipeleka timu hiyo alama moja juu ya vinara wa sasa Atletico Madrid huku mechi tano zikiwa zimesalia kumalizika kwa kandanda ya La Liga, badala yake wanaendelea kushika nafasi ya tatu alama moja nyuma ya Atletico Madrid sawa na Real Madrid.

Mechi ya kibabe ni Jumamosi ya Mei 8, ambapo Barcelona na Atletico Madrid watachuana vikali.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares