Barcelona chali kwa Valencia Kombe la Copa Del Rey

Valencia ndio mabingwa wapya wa kombe la Copa Del Rey. Valencia wametwaa ubingwa huo baada ya kuwafunga FC Barcelona goli 2-1 na hivyo kufanya kuwa msimu mbaya kwa Barcelona baada ya mwezi uliopita kukosa taji la UEFA Champions League, mchezo uliofanyika dimba la Estadio Benito Villamarin Jumamosi, Mei 25.

Barcelona ikimkosa Luis Suarez ilichukua mpira kwenye nyavu zao kwa goli la kwanza lililofungwa na Kevin Gameiro dakika ya 21 kabla ya Rodrigo kuja kumaliza kazi kwa vijana wa Los Ches kipindi cha kwanza.

Goli la kufutia machozi la Barcelona limetiwa kimiani na nahodha wa kikosi hicho Lionel Messi, goli ambalo limelalamikiwa na wachezaji wa Valencia licha ya kutofanikiwa.

Ushindi wa Valencia umemfanya kocha wa Barcelona Ernesto Valverde kushindwa kutwaa makombe mawili ya nyumbani.

Matokeo hayo yanaifanya Barcelona kutwaa ubingwa mmoja tu wa La Liga kwa msimu wa 2018/19 baada ya kuondolewa katika ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool.

Author: Bruce Amani