Barcelona inafanya mazungumzo na Xavi kuhusu nafasi ya kocha

Hatima ya Kocha wa Barcelona Ernesto Valverde inaonekana kuwa kwenye mashaka makubwa baada ya klabu yake kukutana na Xavi wakati kukiongezeka uvumi kuwa nguli huyo wa zamani wa klabu hiyo huenda akatwaa usukani.

Uvumi huo umeshika kasi baada ya klabu ya al-Sadd ya Qatar ambayo Xavi anafundisha, kusema kuwa Barcelona inafanya mazungumzo naye. Mkurugenzi wa spoti wa Al-Sadd Muhammad Ghulam Al Balushi aliiambia televisheni ya Alkass nchini Qatar kuwa kuna mazungumzo kati ya Xavi na Barcelona sasa na wanamtakia kila la kheri popote atakakoamua kwenda.

Xavi amesema alikutana na mkurugenzi wa michezo wa Barcelona Eric Abidal Ijumaa mjini Doha lakini hakufichua aina ya mkutano waliokuwa nao. Alisema hawezi kuficha ndoto ya kuwa kocha wa Barca siku moja lakini kwa sasa yeye anaelekeza nguvu zake kwenye klabu ya Al-Sadd.

Xavi mwenye umri wa miaka 39 alijiunga na Al-Sadd mwaka wa 2015 akitokea Barca baada ya kushinda mataji 17 akiwa na miamba hao wa Uhispania.

Kocha Valvarde yuko chini ya shinikizo kubwa baada ya timu yake kufungw amabao mawili ya dakika za mwisho dhidi ya Atletico Madrid katika kipigo cha 3 – 2 cha nusu fainali ya Kombe la Super Cup la Uhispania. Kipigo hicho kimeongeza mtazamo kuwa timu ya Valverde hutupa uongozi dhidi ya mahasimu wakali, na kuchafua rekodi yake imara ambayo ni pamoja na kushinda mataji mawili ya ligi mfululizo.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends