Barcelona yajiimarisha kileleni baada ya ushindi dhidi ya Vallecano

Klabu ya Barcelona imeendeleza pengo la alama saba kwenye mbio za ubingwa wa La Liga baada ya kupata matokeo ya goli 3-1 dhidi ya Rayo Vallecano siku ya Jumamosi katika uwanja wa Camp Nou.

Rayo walifanikiwa kuongoza dakika 24 tu za Kipindi cha kwanza kupitia kwa Raul de Tomas anayekipiga akitokea Real Madrid kwa mkopo aliyefunga goli bora baada ya makosa ya walinzi wa Barcelona.

Goli la kwanza la Barca alifunga Gerrard Pique lilitokea baada ya makosa ya kumsahau Mlinzi huyo kupitia mpira wa freekick uliopigwa na Lionel Messi

Kipindi cha pili mshambuliaji wa timu hiyo Lionel Messi alifunga goli la pili kupitia mkwaju wa penati uliopigwa naye katika dakika ya 51. Luis Suarez alifunga bao la tatu na la ushindi. Messi anaongoza orodha ya wafungaji mabao katika La Liga akiwa na mabao 26 katika mechi 25. Suarez ni wa pili na magoli 17.

Nambari mbili kwenye msimamo wa ligi Atletico Madrid walipata ushindi wa 1 – 0 dhidi ya Leganes mapema Jumamosi, huku Saul akifunga bao hilo pekee la ushindi.

Author: Bruce Amani