Barcelona yakanusha kukiuka sheria za usajili kuhusu kiungo wa PSG

287

Barcelona imekanusha ripoti kuwa imefikia makubaliano na Paris Saint-Germain ya kumsaini kiungo Adrien Rabiot na wamepuuzilia mbali madai ya kukiuka kanuni zao za biashara ya uhamisho.

Mabingwa hao wa La Liga wamehusishwa na tetesi za kumtaka Rabiot, ambaye mkataba wake na PSG unakamilika mwishoni mwa msimu huu.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alijiondoa kwenye mazungumzo ya kuurefusha mkataba wake na hajajumuishwa katika kikosi cha kwanza za mabingwa hao wa Ufaransa tangu Desemba 5, ijapokuwa kocha Thomas Tuchel anasisitiza kuwa ni uamuzi wa kandanda.

Mkurugenzi wa michezo wa PSG Antero Henrique alidai kuwa Rabiot “aliipotosha” klabu hiyo kuhusu nia yake ya kusaini mkataba mpya na akaituhumu Barca kwa kutofuata sheria za uhamisho akidai kuwa makubaliano ya kabla ya mkataba yalifikiwa na mchezaji huyo nje ya kipindi kinachoruhishwa cha usajili katika miezi sita ya mwisho ya mkataba wake.

Mabngwa wa La Liga wametoa taarifa wakithibitisha kuwa waliwasiliana mara mbili na PSG kuhusu Rabiot lakini wakakanusha kuwepo mpango wowote uliofanyika au kukubaliwa.

“FC Barcelona ingependa kusema kuwa mawasiliano pekee yaliyofanyika ilikuwa Agosti na wiki moja iliyopita. Yalihusu nia ya FC Barcelona kutaka kumsajili Adrien Rabiot”. Ilisema taarifa hiyo.

Author: Bruce Amani