Bayern Munich, Borrusia Dortmund zawapa wapinzani wao vipigo vizito Bundesliga

Bayern Munich imefanikiwa kupata ushindi mnono wa goli 5-0 dhidi ya Eintracht Frankfurt katika mchezo wa Ligi Kuu Ujerumani Bundesliga huku mshambuliaji wa timu hiyo Robert Lewandowski akiandikisha rekodi ya namna yake kwa kupitia bao tatu.

Bayern ambao katikati ya wiki walitoa kichapo cha goli 4-0 dhidi ya Atletico Madrid Ligi ya Mabingwa Ulaya wanaonekana kuimarika siku baada ya siku huku strika huyo akiwa mfungaji wa kwanza kuwa na goli 10 katika mechi tano za mwanzo.

Furaha ya Mabavaria hao huenda isiwe nzuri kwa beki wao wa kushoto Alphonso Davies ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki nane kutokana na majeruhi.

Lewandowski alitangulia kufunga bao, likaja la pili kwa kichwa na goli la mwisho akitumia vyema pasi ya Mbarazil Douglas Costa.

Leroy Sane na Jamal Musiala wamefunga pia kila mmoja bao moja ambapo Bayern inakuwa timu ya kwanza kufunga goli 22 kwenye mechi tano za mwanzo.

Matokeo hayo yanaifanya Bayern kufikisha alama 12 pointi moja nyuma ya vinara RB Leipzig ambao wamemchapa Hertha Berlin 2-1.

Kwingineko, Borussia Dortmund wameichapa timu pinzani ya mji mmoja ya Schalke 04 goli 3-0, magoli ya Manuel Akanji, Erling Braut Haaland na Mats Hummels. Katika matokeo mengine, RB Leipzig iliifunga Hertha Berlin 2 – 1

Author: Bruce Amani